CHADEMA ARUSHA WAZIDI KUMONG'ONYOKA

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Arusha kimeendelea kumeguka baada ya jana vigogo wake wanne wakiwemo wenyeviti wawili wa wilaya kutangaza kujiuzulu nyadhifa zao pamoja na uanachama kutokana na ufisadi unaodaiwa kuwepo ndani ya chama hicho ngazi ya taifa.

Wakitangaza uamuzi huo jana mbele ya waandishi wa habari jijini Arusha Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Monduli, Amani Silanga na Mwenyekiti wa wilaya ya Ngorongoro, Revocatus Parapara walisema baada ya kujiuzulu nyadhifa na uanachama wanatafakari kuona chama gani watajiunga nacho.

Akizungumza wakati wa kutangaza azma hiyo, Silanga alisema amefikia uamuzi huo kutokana na manyanyaso na uvunjaji wa katiba unaofanywa na viongozi wa chama hicho mkoa kwa mashinikizo ya uongozi wa taifa ili kutimiza malengo yao.

Silanga alisema moja ya hatua za uvunjaji wa katiba ni pale alipotangazwa kusimamishwa uongozi na katibu wa chama hicho kanda, Amani Golugwa kufuatia msimamo wake wa kupinga kusimamishwa uongozi kwa naibu katibu mkuu Zitto Kabwe, mjumbe wa kamati kuu Dk Kitila Mkumbo na aliyekuwa mwenyekiti wa wake mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.

Alisema kutokana na msimamo wake huo katibu huyo alitangaza kumsimamisha uongozi pasipo vikao husika kukaa na kumjadili.

Naye mwenyekiti wa wilaya ya Ngorongoro alisema ameamua kujiuzulu nafasi zake hizo kutokana na kutambua kuwa Chadema sio chama cha ukombozi wa kizazi hiki kama wanavyodai kwa kuwa kimeonekana kuwa na maslahi na baadhi ya watu siyo Watanzania.

Alisema hatua za yeye kusimamishwa uongozi na mtu mmoja tu bila vikao kukaa tena kwa madai ya usaliti kwa kukataa kuunga mkono kusimamishwa uongozi kwa Zitto Kabwe na wenzake kulisababisha kukata tamaa na chama hicho.

Alisema kwa muda aliokaa madarakani wilayani humo aliweza kuanzisha matawi ya chama hicho katika kata 20 na kupata wanachama 15,000 ambao kwa sasa wapo nyuma yake kujiunga na chama atakachojiunga nacho yeye kwa maslahi yao na jamii.

Vigogo wengine waliotangaza kujiuzulu nafasi zao za uongozi na uanachama ni mwenyekiti Chadema kata ya Terati jijini Arusha, Gerald Majengo na Katibu mwenezi wa kata ya Olorien, Prosper Mtinanga ambao wote kwa pamoja wamedai kuchoshwa na utapeli na ufisadi wa kisiasa uliopo ndani ya Chadema.

Aidha aliongeza kuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amekuwa akifanya kazi za viongozi wa chama kwa kutangaza kuwafukuza wanachama wanaozungumza ukweli ambapo yeye binafsi aliwahi kupigwa na kutangazwa kufukuzwa uanachama na Mbunge huyo kwa kuhoji tu kiwanja alichopewa na wafadhili kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya akina mama.

Naye Mtinanga alieleza kuwa chama hicho kimekuwa na ufisadi sio wa fedha tu au mali za chama bali hata katika nafasi za uongozi ambazo zimekuwa zikitolewa kwa upendeleo kwa ukabila, ukanda na hata kifamilia, jambo ambalo linaonesha kuwa chama hicho kinaendeshwa kama Saccos.

Mpasuko huu unatokea kipindi ambacho Chadema kimeonekana kuangukia pua vibaya katika chaguzi mbalimbali za marudio za ubunge na udiwani nchini ambapo katika chaguzi za kata 27 Chadema iliambulia kata 3, dhidi ya 23 zilizochukuliwa na CCM wakati kati uchaguzi wa wabunge katika majimbo ya Kalenga na Chalinze CCM iliibuka mshindi kwa asilimia zaidi ya 80.

Comments