DIAMOND AUTIBUA MSAFARA WA RAIS

Stori:IMELDA MTEMA
STAA wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’, Alhamisi iliyopita alijikuta akiutibua msafara wa Rais wa Zanzibar, Dk. Mohamed Shein kufuatia kuondoka kwenye msiba wakati ilitangazwa kiongozi huyo ndiye aliyetakiwa kuanza kuondoka

Ishu hiyo iliyotafsiriwa kama jeuri ya staa huyo ilitokea Mbuzini Mjini Magharibi, Zanzibar baada ya kumalizika kwa mazishi ya baba wa Wema Sepetu, aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania Urusi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Waziri wa Elimu wa zamani katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, marehemu Isaac Abraham Sepetu.

DIAMOND AINGIA
Awali, wakati waombolezaji wamekaa wakiusubiri mwili wa marehemu ufike, ghafla Diamond aliibuka akisindikizwa na kundi la wapambe mpaka alipokaa.

AWEKWA MSTARI WA MBELE
Diamond alipofika aliwekwa mstari wa mbele ambako walikaa ndugu wa karibu na watoto wote wa marehemu.

MC ATANGAZA ITIFAKI YA SERIKALI
Mwili ulipowasili, ratiba ya mazishi ikatangazwa na MC ambapo alitaja utaratibu wa mazishi mpaka watu watakaotakiwa kuweka mashada ya maua kaburini, akiwemo Rais Shein.

Baada ya mazishi, Mwongoza Shughuli ambaye jina halikujulikana aliwaomba watu wote wazingatie itifaki ya usalama wa taifa kwamba ni lazima viongozi wote wa serikali waondoke ndipo waombolezaji wengine watawanyike.

“Jamani naomba sana itifaki izingatiwe, asiondoke mtu yeyote kabla ya viongozi wetu wa serikali, akiwemo Rais Shein hawajaondoka,” alisema MC huyo.

DIAMOND APUUZA, ANYANYUKA
Baada ya MC huyo kutoa mwongozo, watu wote walitulia wakisubiri kiongozi wa kwanza kuondoka ambaye alikuwa ni Rais Shein kama itifaki ilivyotaka.

Lakini kabla Rais Shein hajaanza kusimama, Diamond alinyanyuka na kuzua kasheshe kwa sababu baadhi ya watu, hasa wa umri wake walianza kumkimbilia huku wakikanyagana na kusababisha hali ya taharuki.

MC AWATULIZA WATU
Baada ya watu kuanza kukimbizana hovyo muongozaji wa msiba huo aliwaomba watulie na kusema kuwa wasiogope ila kuna staa ambaye anapita ndiyo maana watu wamemkimbilia.

“Naomba utulivu huyo ni staa f’lani kapita huko ndiyo maana watu wanamkimbilia hivyo tulieni kwanza viongozi wetu waondoke,” alisema.

USALAMA WA TAIFA NUSURA WAMKAMATE
Baada ya kuona watu wakikimbia hovyo baadhi ya maofisa wa usalama wa taifa walitaka kumkamata msanii huyo wakisema alisimama kwa makusudi licha ya kusikia tangazo la kiitifaki.

WATU WAMSHANGAA DIAMOMD
Baadhi ya watu waliohudhuria msiba huo walionekana kushangazwa na kitendo cha Diamond na kusema kuwa ni vyema angesubiri viongozi wote waondoke ndipo na yeye atimke lakini kufanya vile si sahihi.

“Huyu Diamond kwani ana nini? Nakumbuka kwenye msiba wa Kanumba kule Dar pia aliingia kipindi ambacho ilitangazwa kuna kiongozi anakwenda, utaratibu ukatibuka, watu wakawa wanamshangilia yeye,” alisema mtu mmoja aliyetoka Dar kwenda Zanzibar kumzika mzee Sepetu.

Comments