KIOJA cha mwaka kilitokea Jumatano wiki hii katika Mahakama ya Jiji ya Sokoine Drive jijini Dar es Salaam, baada ya mkazi mmoja wa Buguruni, Hassan Omary kujisaidia haja kubwa kizimbani wakati akisomewa shtaka lake la uzururaji.
Mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo, Richard Magodi alikuwa akimsomea shtaka hilo, mbele ya Hakimu Mfawidhi, William Mutaki na alipotakiwa kukiri au kukanusha kosa lake, mtuhumiwa huyo alibaki kimya akiwa amemtumbulia macho hakimu.
Katika hali isiyotarajiwa, mtuhumiwa huyo alionekana akijikamua kama anayejisaidia na ghafla, harufu kali ya kinyesi ikatanda mahakamani hapo.Hakimu alitahayari kufuatia tukio hilo, kwani aliziba pua yake kwa kutumia koti lake na kuuliza chanzo cha mtuhumiwa kufanya kitendo hicho kortini, lakini katika hali iliyoashiria kama ni kiburi, kijana huyo hakujibu chochote zaidi ya kutazama chini, licha ya swali hilo kurudiwa zaidi ya mara tatu.Kutokana na kosa hilo ambalo liliharibu na kusimamisha karibu shughuli zote za mahakama kwa muda, Hakimu Mutaki alimhukumu kijana huyo kwenda jela kwa muda wa miezi sita ili kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia hiyo.
Kana kwamba haitoshi, askari waliokuwepo mahakamani hapo walilazimika kumchapa bakora kijana huyo ili kumlazimisha kupiga deki baada ya eneo hilo kuchafuka vibaya kwa kinyesi kilichochanganyika na mkojo.
Comments
Post a Comment