Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimelishutumu kwa Jeshi la Polisi kwamba wafuasi wa chama hicho wanaokamatwa kwa makosa mbalimbali, wamekuwa wakishinikizwa watamke kuwa wametumwa na viongozi wao waandamizi kufanya vitendo hivyo. Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema wafuasi wa chama hicho walioshinikizwa ni wale waliokamatwa na polisi hivi karibuni wakihusishwa na kummwagia tindikali kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Tesha, tukio lililotokea mwaka 2011.
Mnyika aliwataja waliokamatwa kuwa ni Oscar Kaijage, aliyekamatwa mkoani Shinyanga, Seif Magesa Kabuta, ambaye alikamatwa mkoani Mwanzai, Evodius Justinian, alitiwa mbaroni mkoani Kagera na Henry Kilewo, ambaye alikamatwa jijini Dar es Salaam.
Alisema wafuasi hao baada ya kukamatwa wameshinikizwa kusema kuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa; Mkurugenzi wa Sheria na Katiba wa Chama hicho na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Mbuge wa Ubungo, John Mnyika kuwa ndiyo waliowatuma kutenda kosa hilo.
Alisema Evodius Justinian, alikamatwa mjini Bukoba na baadaye akapelekwa mkoani Mwanza na kuletwa jijini Dar es Salaam ambako amefichwa hadi sasa hajulikani aliko.
Mnyika alisema taarifa za kada huyo kuletwa Dar es Salaam zilikuwa za kificho kwani wakili wake Nyaronyo Kicheere, akiongozana na ndugu wa mtuhumiwa huyo walifika Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na kuelezwa kuwa amepelekwa makao makuu.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, alipotafutwa jana hakupatikana kutokana na simu yake kuita bila kupokelewa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi, alipoulizwa alithibitisha mtuhumiwa huyo kukamatwa baada ya kupewa taarifa kutoka makao makuu kwamba amefanya kosa Igunga ambako walimsafirisha kumpeleka huko.
Kamanda Kalangi alisema taarifa za kwamba baada ya kukamatwa alishinikizwa awataje viongozi wake waandamizi, hafahamu kama Jeshi la Polisi linaweza kufanya hivyo.
“Polisi hatuwezi kulenga mwanachama wa chama fulani, tunashughulika na wahalifu,” alisema.
Mnyika alisema mtuhumiwa wa pili ni Seif Magesa Kabuta aliyekamatwa Mwanza ambaye baada ya kukataa kukiri kuwa viongozi wake wanahusika na matendo hayo, walimfungia katika chumba maalum wakamleta mke wake, mama yake mzazi na mkwe wake na kumtesa mbele yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa Mwanza, Ernest Mangu, alisema hana taarifa za kada huyo wa Chadema kwamba alikamatwa katika mkoa wake.
“Kwanza taarifa za kwamba huyo Seif Kabuta, tulimkamata Mwanza sina na kwasababu hiyo siwezi kuwa na majibu kama analazimishwa kuhusika na tukio la kummwagia tindikali kada wa CCM,” alisema.
Mtuhumiwa wa tatu aliyekamatwa mkoani Shinyanga kwa kuhusishwa na tukio hilo la tindikali ni Oscar Kaijage.
Mnyika alisema baada ya mtuhumiwa huyo kukamatwa, awali aliambiwa ni kwa sababu kuna fedha zimepotea kwa njia ya simu na yeye alikuwa anajishughulisha na uwakala wa fedha kwa njia ya mitandao ya M-Pesa, na Z-Pesa.
Alisema baadaye alipokutanishwa na makachero wa polisi makao makuu, alielezwa kuwa amekamatwa kwa kosa la kuhusika na tukio la kummwagia tindikali kada wa CCM, Mussa Tesha.
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Evarist Mangala, alipoulizwa alisema hana taarifa za kumatwa mtu huyo kutoka katika mkoa huo.
Mtuhumiwa wa nne ni Rajab Kihawa, ambaye anadaiwa kupigiwa simu na mwanamke asiyemfahamu na baadaye akakutanishwa na maofisa wa polisi ambako anadaiwa aliombwa akubali kupewa Sh. milioni 30 ili akubali kusema kuwa Mbowe na wenzake waliwatuma kummwagia tindikali Tesha.
Mtuhumiwa wa mwisho ni Henry Kilewo, Katibu wa Chadema wa Wilaya ya Kinondoni na Katibu wa Makatibu wa Chadema Kanda Maalum ya Dar es Salaam ambaye anadaiwa aliitwa Polisi bila kuambiwa anakwenda kuhojiwa juu ya suala gani.
Hata hivyo, alipofika makao makuu ya Polisi alidai walisita kumwambia, lakini walishauriana baadaye wakamwambia anatuhumiwa kummwagia Tesha tindikali.
BY THOBIAS MWANAKATWE
SOURCE: NIPASHE
Comments
Post a Comment